Mbunge wa eneo bunge la Mugirango Kusini Manson Nyamweya amesema haijalishi kiwango cha pesa makamishena wa tume ya uchaguzi nchini IEBC watalipwa ikiwa watasimamishwa kazi bora kuwa na haki, uwazi na amani katika uchaguzi mkuu ujao.
Hii ni baada ya kubainika kuwa ikiwa makamishina hao wa IEBC watasimamishwa kazi huenda walipwe pesa nyingi kwa kukatizwa kwa mkataba wao kabla ya wakati wake, pesa hizo zinakadiriwa kuwa zaidi ya shillingi millioni mia nne.
Akizungumza mjini Kisii, Mbunge Nyamweya alisema amani ni muhimu kuliko pesa akisema makamishina hao waondolewe pasi kujali kiwango cha pesa watakazofidiwa.
“Tunajua kuwa makamishina wa IEBC wakiondolewa watalipwa pesa kwa mda ambao umesalia lakini hilo si jambo la muhimu tunataka waondolewe na tuwe na wengine wapya bora kuwe na amani katika taifa letu la Kenya,” alisema Nyamweya.
Wakati huo huo, Nyamweya alisema maandamano ya muungano wa Cord yamezaa matunda kwani serikali imekubali kuwa na mazungumzo na upinzani.
“Maandamano ya upinzani yameonekana kuleta matunda katika taifa letu dhidi ya kuwaondoa makamishina wa IEBC kwani serikali imekubali mazungumzo na upinzani na tunahitaji IEBC iende nyumbani,” aliongeza Nyamweya.