Huku michezo ya shule za sekondari iking’oa nanga rasmi katika kaunti ya Kisii, kibarua cha kuwasafirisha wanafunzi kushiriki michezo hiyo kimeonekana kufuatia ukosefu wa mabasi katika shule za eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini.
Sasa wakazi wa eneo bunge hilo wamehimiza mbunge wa eneo hilo Jimmy Angwenyi kuzinunulia baadhi ya shule za upili mabasi ya kuwasafirisha wanafunzi hao.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika eneo la Marani, idadi kubwa ya wakazi hao walisema kuwa ukosefu huo wa mabasi hulazimu wanafunzi kutumwa nyumbani kuleta pesa za kukodisha mabasi kuwasafirisha, jambo ambalo huwakera wazazi kwani linaendelea kushuhudiwa kila mara
Angwenyi ameombwa kujali maslahi na kupunguzia wazazi mzigo na kununulia baadhi ya shule za upili za eneo hilo mabasi, haswa zile ambazo zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na katika michezo mbalimbali.
“Baadhi ya shule katika eneo hili hufanya vizuri katika michezo na katika mitihani, na zinastahili kuwa na mabasi kupitia mbunge wetu ili kurahisisha usafirishaji wa wanafunzi haswa katika michezo hiyo ,” alisema John Araka, mkazi pia mzazi wa shule ya Rioma.
Miongoni mwa shule ambazo wakazi hao walipendekeza kununuliwa mabasi ambazo hufanya vyema katika michezo na masomo ni Eramba, Rioma, Nyagesenda, Tambacha, na Marani.
Picha: Mbunge Jimmy Angenyi (katikati). Amehimizwa kununulia shule mabasi zinazofanya vyema kimasomo na michezo katika eneo bunge lake. Makataba