Mtunga sheria mmoja mjini Nakuru ameshtumu kitendo cha wabunge wa ODM kupiga kelele wakati rais Uhuru Kenyatta akihutubia taifa, ambapo alikitaja kama “cha kijinga”.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge huyo vile vile alimkashifu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kuwatetea wabunge hao saba.

“Odinga ambaye ni kiongozi wa chama cha ODM na muungano wa CORD, sasa amekumbatia mienendo potovu ya wabunge wake, na kuanza kuwatetea. Kitendo chao hicho mbele ya rais na taifa, kilikuwa cha kijinga,” alisema mbunge Samwel Arama.

Samwel Arama wa Nakuru Magharibi aidha amekanusha madai ya kuwasafirisha wapigaji kura katika eneo lake la ubunge ili wajisajili katika eneo hilo, kwa lengo la kupata wingi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao 2017.

Arama amesema “waliofanya hivyo walijitakia wenyewe kubadilisha vituo vya kupigia kura kama ilivyotangazwa na IEBC”.

“Kila mkenya ana haki ya kikatiba ya kuchukua kura mahala popote nchini Kenya,” akasema mbunge huyo.

Arama alisema hayo Jumanne mjini Nakuru wakati akipuzilia habari zilizotolewa na mwenyekiti wa bodi ya maji ya mkoani bonde la uffa (RVWSB) John Kitilit, akisema kumekuwa na ongezeko la watu kutoka nje ya eneo bunge hilo waliojiandikisha, haswa katika zoezi lililotamatika mwezi Marchi la uandikishaji wa wapiga kura.

Arama ambaye ameasi chama cha ODM na kutangaza nia ya kutetea kiti chake kwa muungano wa Jubilee amewarai wakaazi katika eneo la bonde la ufa kuungana pamoja na kusimama na muungano huo.