Mbunge wa Nakuru mjini Magharibi Samuel Arama ametoa wito kwa mrengo pinzani wa Cord kuheshimu sheria na serikali ya Jubilee iliyochaguliwa na mwananchi.
Katika kikao na wanahabari mjini Nakuru, Arama alisema kuwa kando na changamoto zilizopo katika taifa, serikali iliyopo yafaa kuheshimiwa na kila mmoja pasi na kujali mirengo ya kisiasa au hata maoni tofauti.
"Hata kama haumpendi Rais Uhuru Kenyatta au naibu wa Rais William Ruto lakini twafaa tufahamu kwamba hiyo ndio serikali iliyochaguliwa na lazima tuiheshimu kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya mwananchi kufanya maamuzi mengine," alisema Arama.
Ametoa wito kwa taasisi husika serikalini kuhakikisha kwamba zinawachukulia hatua kali viongozi wanaoeneza siasa za ukabila na uchochezi katika mikutano ya hadhara na hasa uchaguzi mkuu unapokaribia.
Wakati uo huo, Mbunge huyo wa Nakuru Magharibi aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM aliongeza kuwa hata kama ametangaza kuhamia Jubilee bado anaheshimu chama cha ODM na upinzani kwa jumla na ni wajibu wa upinzani pia kuhakikisha unaheshimu serikali.
Kwa mujibu wake atazidi kushirikiana na serikali ya Jubilee ili kuleta maendeleo katika eneo bunge lake la Nakuru Mjini Magharibi.