Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama ametaka viongozi wa serikali waliotajwa kwenye kashfa ya ufisadi ya shirika la NYS kubeba misalaba yao wenyewe.

Akizungumza kwenye Shule ya msingi ya Nakuru Magharibi siku ya Ijumaa, Arama alisema kuwa waliotajwa katika kashfa za wizi wa fedha za serikali wanafaa kulimbikiziwa lawama hizo na wala sio kwa watu kuhusisha Rais Uhuru Kenyatta na wizi wa fedha hizo.

“Kama wewe umeiba pesa ya serikali, unafaa kufanyiwa uchunguzi kama mtu binafsi. Tusianze kuchafulia Rais Kenyatta jina kwa kusema kuwa alikuwa anajua kuwa pesa za umma zimeibiwa,” alisema Arama.

Wakati huo huo, aliwahimiza wakaazi wa Nakuru kuwachagua viongozi kwa misingi ya kazi ambayo wametekeleza.

“Tunataka ikifika wakati wa kura mpigie kura yule kiongozi ambaye atawasaidia. Kama mtaona kuwa kiongozi huyo ni Arama, basi mumpigie kura na mkiona Arama hawezi, wachana na yeye,” alisema mbunge huyo.

Alisisitiza kuwa wakaazi wa Kaunti ya Nakuru wanafaa kutozingatia vyama katika kuwachagua viongozi katika uchaguzi mkuu ujao na badala yake kuzingatia viongozi hao walivyowatumikia wananchi.

“Kama umeona Arama amefanya kazi nzuri, usimwambie aende katika chama cha ODM, TNA au aende katika chama chochote kile ili umchague. Chagua Arama kulingana na ile kazi ambayo ameitenda,” alisema Arama.