Mbunge wa Nakuru mjini magharibi Samuel Arama kwa mara nyingine tena ameshtumu baadhi ya wabunge wa ODM waliomkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta wakati wa hotuba kwa taifa kwa kupuliza firimbi.
Akizungumza katika mazishi ya Charles Bowen katika wadi ya Kapkures eneo Bunge la Nakuru Mjini Magharibi, Arama alisema kuwa Taasisi ya Rais inafaa kuheshimiwa.
"Hata kama hawampendi Rais Kenyatta binafsi wanafaa kuheshimu taasisi ya Rais kwani hata Raila akiwa kwa taasisi hiyo atataka heshima,"alisema Arama.
Aliongeza kuwa upinzani una wajibu wa kuikosoa serikali lakini wanafaa kufanya hivyo kwa ustaarabu fulani.
Mwendazake Bowen alikuwa mwenyekiti wa KANU wadhifa aliyoshikilia hadi kufa kwake.
Ni hafla iliyohudhuriwa pia na mwenyekiti wa mamlaka ya usalama barabarani NTSA Lee Kinyanjui ambaye alisisitiza kwamba atakuwa kinyanganyiro cha ugavana Nakuru 2017.
Naye Gavana Kinuthia Mbugua aliwakilishwa na Naibu wake Joseph Ruto ambaye alitoa wito kwa wanasiasa kuhubiri amani.