Mbunge wa Nakuru mjini Magharibi Samuel Arama amesema kuwa ana hakika ya kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili kama mbunge wa eneo hilo kutokana na rekodi yake ya maendeleo.
Arama amesema kuwa wapiga kura wa eneo hilo watamchagua tena kwa kura nyingi hata zaidi ya zile walizompigia mwaka 2013.
Akiongea Jumatano mtaani kaptembwo Arama alisema kuwa yuko tayari kumenyana na wapiznani wake na kuwaonyesha kivumbi katika uchaguzi mkuuu ujao.
Aliongeza kuwa wapiga kura wa Nakuru mjini magharibi walimpa wajibu wa kutekeleza mwaka 2013 na ameutekeleza ipasavyo.
“Mimi niliomba kazi mwaka 2013 na watu wa Nakuru Magharibi wakanipa kura na mimi nimefanya kile walinituma kufanya na bado najua mwaka 2017 watanipa kazi tena,” alisema Arama.
“Mimi nikitembea, nikikaa na hata nikilala sina wasiwasi hata kidogo kwa sababu najua kazi yangu iko salama,” aliongeza.
Arama aidha alisema kuwa haogopi kupitia mchujo wa chama cha Jubilee na kusema kuwa ana uhakika wa kushinda mchujo huo.
“Watu wengine wanasema kuwa ati sitatoboa mchujo wa Jubilee lakini watashangaa wakiona Arama akiwa huko mbele na wao wakifuata,” alisema.
Arama ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM katika uchaguzi uliopita ametangaza kuhamia chama cha Jubilee atakachotumia kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao.