Askari wa Kaunti ya Nyamira waliosimamishwa kazi wameupinga ombi la Serikali ya Kaunti hiyo kuwahitaji kuzirudisha sare zao za kazi walizopewa hapo mbeleni.
Wakizungumza na Wandishi wa habari siku ya Jumatano katika mji wa Nyamira, wafanyikazi hao sasa wanataka haki itendeke kwa kupata suluhu mwafaka unaozingira kesi yao.
Mkuu wa Idara ya fedha katika Kaunti ya Nyamira John Omanwa amekanusha madai hayo ya kusema wanakandarasi walioajiriwa na Serikali ya kaunti hiyo ya Nyamira wamefutwa kazi ila wamesimamishwa kazi kufuatia wakati wao waliopatiwa kufanya kazi kama wanakandarasi kufika mwisho.
Aidha, Omanwa alisema watu huajiriwa katika kaunti hiyo kwa muda kati ya miezi mitatu hadi sita na watu hao pia kutafuta ajira upya kufuatia sheria za Serikali ya kaunti hiyo.
“Mtu hupata kandarasi ya kufanya kazi kati ya miezi mitatu hadi sita na muda wa kandarasi ukimalizika watu hujiandikisha upya,” alisema Omanwa.
“Haya mambo watu wanashinda wakisema kwamba wamefutwa kazi ni uongo maanake muda wao ndio umefika mwisho kama ilivyo kwenye mkataba kati yao na Serikali ya Kaunti ya Nyamira,” aliongeza Omanwa.
Askari hao hata hivyo wamesimama kidete kwa kusema hawatarudisha sare zao ila kutendewa haki kama wakaazi wa kaunti hiyo.
“Baada ya muda wa mfanyikazi kufika mwisho inafaa kujiandikisha upya jinsi Serikali yetu ilisema hapo mbeleni, sio kupiga domo kama hao wenyewe ndio hawakujiandikisha upya na kusema hawatarudisha sare za kazi,” alisisitiza Omanwa.