Askari wawili wa Kaunti ya Mombasa wanazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central Mjini Mombasa baada ya kutiwa nguvuni hapo jana wakikabiliwa na makosa ya ufisadi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mkuu anayesimamia Askari hao Charles Changawa amesema kwamba Askari hao wanadaiwa kuzuru hoteli ya ‘Vipingo Rigde golf resort’ huko vipingo katika kaunti ya Kilifi na kuchukua hongo kutoka kwa msimamizi mkuu wa hoteli hiyo Peter Oluoch.

Kulingana na Changawa imewabidi Askari hao kuwekwa kwenye gwaride katika chuo cha mafunzo ya askari katika eneo la Tudor ili kumpatia nafasi mfanyibiashara huyo kuwatambua wale wanaozuru katika hoteli hiyo ili kuchukua hongo.

"Serikali ya kaunti ya Mombasa kamwe haiwezi kuruhusu ufisadi kufanyika katika idara mbalimbali kaunti hiyo na watakapatika lazima watachukuliwa hatua za kisheria," alisema Changawa siku ya Alhamis katika afisi za idara hiyo eneo la Tudor.

Oluoch ameweza kuwatambua wawili katika ya askari ambao wamekuwa wakikusanya hongo angalau mara tatu kwa wiki katika hoteli hiyo na ambao Changawa ameamuru watiwe nguvuni na kuzuiliwa kadri uchunguzi zaidi unavyoendelezwa.

Wakati uo huo, Changawa amewasihi wakaazi wa kaunti hiyo ya Mombasa kuwaripoti Askari wafisadi au wale wanaowahangaisha Wakaazi katika Kaunti hiyo, ili wachukuliwe hatua huku akisisitiza kwamba wale watakopatikana na hatia watafutwa kazi.