Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Askofu wa jimbo katoliki la Nakuru Maurice Muhatia Makumba anasisitiza kwamba majadiliano ndio njia ya kipekee ya kuafikia mwafaka utakaopelekea kusitishwa kwa mgomo wa walimu.

Muhatia ambaye pia ni mwenyekiti wa tume inayoshughulikia maswala ya elimu na elimu ya kidini katika baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki hapa nchini KCCB amehoji kwamba bado hakujakuwa na majadiliano ya kutosha kuafikia uamuzi wa shule kufungwa.

"Katika nchi yetu kuna mvutano kwenye sekta ya elimu kwani upande mmoja kuna waaalimu wanaotaka kuongezwa mshahara. Upande mwingine serikali inasema hakuna pesa na kwa upande mwingine, mahakama imefanya uamuzi wa waalimu kuongezewa mishahara. Sisi tunasema hakujakuwa na majadiliano ya kutosha kusababisha shule zifungwe," amesema askofu Muhatia.

Kwenye mahubiri ya misa katika parokia ya St John and Paul Kamwaura viungani wa mji wa Nakuru, wanafunzi ambao wamelazimika kusalia nyumbani kutokana na agizo la serikali la kufungwa kwa shule zote ndio wanaoumia.

Askofu Muhatia aidha anakariri kwamba licha ya shule kufungwa, haziwezi kusalia zikiwa zimefungwa kwa muda mrefu na ni kutokana tu na majadiliano ambapo mwafaka utaafikiwa.

"Tunaendelea kusihi serikali na waaalimu wajadiliane kwani hakuna njia nyingine, tupende tusipende. Shule haziwezi kufungwa mpaka Desemba mwaka ujao, lazima zitafunguliwa," alikariri Askofu Muhatia.