Askofu Mkuu wa Kanisa la African Brotherhood Church (ABC) nchini Timothy Ndambuki amehimiza wazazi kuzingatia elimu ya wanao akisema kuwa masomo ndio zawadi ya kipekee ya mzazi kwa mwanawe.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye kikao cha Elimu na Maendeleo na viongozi wa dini ya Got Calvary Legion Maria Church katika makao makuu ya Kanisa hilo, St Joseph Thim Maseno katika Kaunti ya Kisumu, Askofu Ndambuki aliwataka viongozi hao kuwasaidia waumini wao kuanzisha miradi ya maendeleo miongoni wao, ili kuweza kumudu gharama za masomo ya watoto wao.

“Nawasihi sana viongozi wa kanisa tena kama wawakilishi wa imani ya waumini, kwamba mzingatie elimu ya watoto wenu mkielewa kuwa ndio zawadi ya kipekee ya maisha bora ya siku zao za baadaye,” alisema Askofu Ndambuki.

Askofu huyo alihoji kwamba kwa kujali kwake maisha ya baadaye ya waumini wa kanisa lake la ABC, aliweza kuanzisha taasisi ya Sayanzi na Ufundi yenye malipo nafuu, kwa malengo ya kuwasaidia wana wa waumini kote nchini kupata elimu.

Alisema kuwa taasisi hiyo inawalipia nusu ya karo watoto wa kutoka jamii za makanisa yaliyojisajili na muungano wa Makanisa Huru ya Kiafrika nchini (AIC), ambayo yeye ni Mwenyekiti wake.

Pia alihoji kuwa wamo mbioni kuanzisha Chuo Kikuu kilichopendekezwa Mjini Machakos mwakani. Mkuu huyo wa kanisa yumo kwenye safari ya siku nne katika Kaunti ya Kisumu ambapo anahamazisha makanisa yaliyo kwenye eneo hilo kuhusu mbinu thabiti za kusitawisha masomo na maendeleo miongoni mwa makanisa.