Mwakilishi wadi ya Gesima Ken Atuti amewaomba mbunge wa Borabu Ben Momanyi na mwenzake wa Kitutu Masaba Timothy Bosire kushirikiana kukarabati shule moja ya msingi iliyoko katika eneo la mpaka wa maeneo bunge hayo mawili.
Akiongea wakati alipoitembelea shule hiyo ya Nyansimwamu, Atuti alisema kuwa kwa muda mwingi, viongozi hao wawili hawajakuwa wakiitikia mwito wa kukarabati shule hiyo iliyoko katika hali mbaya, huku akiongezea kuwa juhudi zake na mwakilishi wa wadi ya Nyansiongo kushinikisha afisi za ustawishaji wa maendeleo bunge hayo mawili hazijazaa matunda.
“Ningependa kuwaomba wabunge Timothy Bosire na Ben Momanyi kushirikiana ili kukarabati paa za shule hii ambazo zimechanika na hali mbaya ya madarasa yanataka kuanguka,” alisema Atuti.
Kulingana na mwakilishi huyo, viongozi hao wawili wanastahili kuchukua hatua za haraka kwa kuwa shule hiyo iko kwenye ardhi ya Borabu na kwenye himaya ya uongozi wa Kitutu Masaba Masaba, swala alilosema kuwa pia linaathiri shule ya msingi ya Nyaronge.
"Hii sio mara ya kwanza kwa swala hili kuchipuza kwa kuwa hata shule ya Nyaronge imejipata katika hali sawa na hii, ila inafaa shule yeyote ile iliyo na mshikamano flani na eneo bunge lolote ifuzu kufadhiliwa na pesa za ustawishaji maeneo bunge,” alisema Atuti.
Wakati wa hafla hiyo, Atuti alifungua rasmi madarasa mawili ambayo yamekuwa yakijengwa na serikali ya kaunti ya Nyamira.