Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amewahakikishia wafanyibiashara katika Soko la Kongowea kuwa jumba la kibiashara katika soko hilo litakamilishwa hivi karibuni.

Jumba hilo lililoko katikati mwa soko hilo linadaiwa kujengwa miaka mingi iliyopita na kuachwa bila kukamilika.

Mbunge huyo alisema kuwa jumba hilo lina umuhimu mkubwa katika soko hilo lenye wafanyibiashara wengi na kuahidi kwamba litakapokamilika, litasaidia kuimarisha biashara zaidi.

Akiongea na wakaazi katika soko hilo siku ya Jumamosi, Awiti alisema kuwa atahakikisha kuwa mpango huo unaanza kutekelezwa katika kipindi cha miezi minne.

“Hili jumba limekaa hapa kwa zaidi ya miaka kumi. Mimi nawahakikishia kuwa nitakamilisha ujenzi huo ili wafanyibiashara waanze kutumia jengo hilo,” alisema Awiti.

Mbunge huyo alisema kuwa sababu ya jumba hilo kukaa miaka hiyo yote bila kukamilika ni kutokana na ufisadi na njia za magendo ambazo zimelemaza shughuli hiyo.

Aidha, alisema kuwa kazi hiyo itapewa vijana wa huduma kwa taifa NYS ili kuona kwamba vijana hao pia wamepata ajira na kujinufaisha.

Aliongeza kuwa hakuna njia za magendo zitakazotumika katika shughuli hiyo, na kusema kuwa wafanyibiashara wanaofanya biashara katika soko hilo watapewa nafasi ya kwanza katika kuendesha shughuli zao hapo.

“Hakutakuwa na magendo eti mtu anaambiwa atoe shilingi elfu mia moja ndio apate nafasi. Mimi nitasimama kitede kabisa,” aliongeza Awiti.

Soko la Kongowea ndilo soko kubwa zaidi mjini Mombasa na linategemewa na watu wengi sio tu mjni humo, bali Pwani kwa jumla.