Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ameomba usaidizi wa wazee wa jamii ya Mijikenda katika jitihada zake za kumng'atua Gavana Hassan Joho katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akizungumza alipokutana na wazee kutoka maeneo bunge sita, Bwana Awiti, alimshtumu Joho kwa kushindwa kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.
Mbunge huyo aliwaomba wazee hao kumuunga mkono katika kuleta maendeleo Mombasa.
"Kwa muda mrefu sasa, jamii ya Mijekenda imekuwa ikitengwa wakati wa kufanya maamuzi kuhusu serikali ya kaunti. Hata hivyo, wakati umefika kwa jamii hii kuungana na kuchangia katika maswala ya uongozi,” aliema Bwana Awiti.
Mbunge huyo aidha aliwarai wazee hao kumchagua mgombea mwenza ambaye atakuwa makamu wake iwapo atachaguliwa kuwa gavana wa Mombasa.
Mbunge huyo pia aliahidi kuimarisha utoaji wa huduma kwa wakaazi wa Mombasa.