Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amekanusha madai ya ufujaji wa takriban shilingi milioni 21 kutoka kwa hazina ya eneo bunge hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wakaazi katika eneo la Ziwa la Ng’ombe huko Bombolulu, Awiti alikemea vikali madai hayo na kusema kuwa fedha hizo zinazodaiwa kupotea zilikuwa katika hazina ya Kisauni, kabla ya Nyali kuteuliwa kuwa eneo bunge.

Kauli hii inajiri baada ya orodha ya majina ya wabunge wanaodaiwa kuhusika katika kashfa za ufisadi kuchapishwa magazetini.

“Inaonekana kuna baadhi ya watu wenye njama ya kutaka kunichafulia jina, lakini nawahakikishia sijahusika katika kashfa yoyote ya ufujaji wa fedha za umma,” alisema Awiti.

Mbunge huyo alisema kuwa yuko tayari kufanyiwa uchunguzi iwapo amehusika katika madai hayo.

Alimtaka mkaguzi mkuu wa fedha za umma nchini kutekeleza uchunguzi wa kina na kutatua kitendawili cha kupotea kwa fedha hizo na kuwataja waliohusika.

“Mkaguzi mkuu wa fedha za umma afanye uchunguzi na awataje waliohusika katika kupotea kwa fedha za umma, wala sio kukaa na kuchafulia watu jina,” alisema Awiti.

Eneo la Nyali lilikuwa chini ya eneo bunge la Kisauni mpaka wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013.