Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amemkashifu Gavana wa Mombasa Hassan Joho kwa kuweka mabango yenye picha zake kuashiria miradi aliyoyatekeleza.
Awiti alisema kuwa tabia hiyo inapaswa kusitishwa na kuitaja kama uharibifu wa mali ya umma.
Mbunge huyo alisema kuwa hamna haja ya kuweka mabango kwa vile hayana manufaa yoyote kwa wananchi.
“Hakuna haja ya kuharibu fedha za umma kwa kuwa wakaazi wanaweza kujionea na kutambua miradi ya maendeleo inapozinduliwa,” alisema Awiti.
Akiongea mjini Mombasa, Awiti alisema kuwa fedha hizo zinazotumika katika kuweka mabango hayo zinaweza kutumika katika kutekeleza miradi mingine kinyume na vile zinavyotumika kwa sasa.
“Hamna haja ya kuweka mabango kuonesha miradi, maendeleo yanaonekana, huo ni ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema Awiti.
Mbunge huyo na viongozi wengine katika Kaunti ya Mombasa akiwemo Seneta Hassan Omar wamekuwa mstari wa mbele katika kukosoa mbinu hiyo ya kuweka mabango.