Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuboresha na kupanua soko la Kongowea zaidi kwa manufaa ya wafanyabiashara.
Awiti amesema kuwa wananchi wengi wa eneo bunge la Nyali wanategemea soko hilo katika kupata riziki na kujikimu kimaisha.
Akizungumza siku ya Jumatano kwenye ufunguzi wa Soko la Kongowea, uliongozwa na Raisi Kenyatta, Awiti aidha alimpongeza rais kwa kutimiza ahadi yake ya kujengwa kwa jengo jipya katika soko hilo.
“Nakuomba mweshimiwa rais uweze kuboresha na kupanua soko hili la Kongowea zaidi,” alisema Awiti.
Aidha, alimpongeza Kenyatta kwa kuweka tofauti za kisiasa kando na kutumika wananchi wa taifa bila ubaguzi.
“Raisi ameonyesha mfano mzuri wa kuweka tofauti za kisiasa kando na kuanza kutumikia wananchi wa tabaka zote nchini,” alisema Awiti.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alionya dhidi ya kuingiza ukabila katika ugavi wa nafasi kwa wafanyabiashara katika jengo hilo jipya.
Rais ameutaka usimamizi wa soko hilo kutumia sheria na usawa katika ugavi huo, ili kila mwananchi anufaike.
Aidha, ameongeza kuwa kila kabila lina haki ya kufanya biashara katika kila pembe ya taifa la Kenya.
Kenyatta pia ameahidi kuboresha na kupanua soko hilo iwapo wafanyabiashara wengine hawatapata nafasi katika jengo hilo.
“Serikali iko tayari kupanua soko hili na kulifanya la hadhi ya juu zaidi,” alisema Uhuru.