Hisia mbalimbali zinazidi kuibuka mjini Mombasa kutokana na visa vya washukiwa wa uhalifu kuuawa na maafisa wa polisi.
Hali hii imewafanya baadhi ya viongozi eneo hilo kujitokeza na kutoa maoni yao kuhusiana na matukio hayo.
Wiki iliyopita, Gavana Hassan Joho pamoja na Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba walikashifu mauaji hayo na kuyataja kama ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amewataka maafisa wa polisi kuanzisha msako dhidi ya wahalifu wanaowahangaisha wakaazi.
Akizungumza na wanahabari katika soko la Kongowea siku ya Jumatano, Awiti aliwakashifu baadhi ya viongozi kwa kusema kuwa hakuna mtu anafaa kupinga oparesheni ya polisi dhidi ya magaidi.
“Ikiwa polisi wamemkamata mtu, ni vizuri wafanye uchunguzi ili kubaini ukweli. Tuwapatie polisi nafasi ya kufanya kazi yao ya kupambana na magaidi,” alisema Awiti.
Mbunge huyo amewakosoa baadhi ya viongozi wanaowahifadhi wahalifu, akisisitiza kwamba wanafaa kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Viongozi hao wanafaa kukamatwa kwa sababu hawako juu ya sheria. Tunataka taifa ambalo kila mtu anafurahia maisha,” aliongeza.
Hata hivyo, amewashauri maafisa wa polisi kufanya uchunguzi wa kutosha badala ya kumpiga mshukiwa risasi.
Haya yanajiri siku chache baada ya polisi kuwaua washukiwa wawili wa ugaidi eneo la Kisauni.