Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amewataka wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao katika mtaa wa Leisure kutoondoka eneo hilo na wajenge tena vibanda vyao.

Awiti aliyasema haya siku ya Jumamosi alipokuwa akiandamana na kundi la vijana kupinga ubomoaji huo, huku akisema kuwa wana haki ya kufanya biashara yao eneo hilo hadi sheria itakapofuatwa ya kuwaondoa mahali hapo.

Awiti aliitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuja na mbinu mbadala ya kusuluhisha tatizo, wala si kubomaoa vibanda vya wafanyibiashara ikizingatiwa ni walipa kodi.

Aidha, aliongeza kuwa wakazi hao hawakupewa ilani ya kuhama katika sehemu hiyo, jambo alilolitaja kuwa kinyume cha sheria.

Vilevile, Awiti alionyesha kughadabishwa jinsi ubomozi huo unavyofanyika, licha ya yeye kushauriwa kama mbunge wa eneo hilo.

Kulingana na wafanyabiashara hao wa eneo la Leisure, vibanda vilibomolewa mwendo wa saa tisa alfajiri bila ya kupewa ilani wala sehemu mbadala ya kufanya biashara.

Wachuuzi hao wa nguo na vyakula walidai kuingia hasara na pia mali yao nyengine kuporwa.