Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Malipo duni pamoja na ukosefu wa marupurupu kwa vikosi vya usalama haswa maafisa wa polisi yametajwa kuwa visababishi vikuu vya ufisadi miongoni mwa maafisa wa usalama.

Viongozi wa eneo la Pwani wamependekeza idara ya polisi kupewa kipaumbele katika kulipwa kwa mishahara mizuri pamoja na marupurupu ya kuridhisha ili kuwaepusha walinda usalama na tabia za ulaji rushwa katika shughuli zao za kila siku.

Akiwahutubia wakaazi pamoja na viongozi mbali mbali wa kisiasa waliokusanyika siku ya Jumamosi katika hafla ya kuadhimisha siku kuu ya Jamhuri, mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bolo, alisema kuwa sharti serikali kuu iweze kuliangalia suala hilo kwa jicho la ndani na kuhakikisha kuwa maafisa wa polisi wanalipwa vizuri ili kuwapa motisha wanapotekeleza kazi zao.

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha CORD alisistiza msimamo wa chama chao kuona kuwa zimwi linaloandama serikali la ufisadi linatokomezwa kwa njia zote na kwa ushirikiano baina na matawi yote ya serikali pamoja na viongozi wenye nia nzuri.

Awiti pia alichukua nafasi hiyo na kupatana na gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, huku akitangaza kuwa kushirikiana na Joho kuna manufaa ya kuletea wakaazi wa kaunti maendeleo.