Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ameahidi kumaliza matatizo ya wakaazi wa Mombasa kwa siku 90 iwapo atachaguliwa kuwa gavana wa Mombasa.

Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo la Changamwe, Awiti alisisitiza kuwa atatatua matatizo yanayowakumba wakaazi wa Mombasa kama vile mizozo ya ardhi, ukosefu wa usalama na ajira, na mizozo ya kibiashara chini ya miezi mitatu baada ya kuapishwa kwake.

Awiti amewataka wananchi kumpigia kura ili kubadilisha sura na uongozi wa eneo la Mombasa, kinyume na jinsi serikali ya sasa ya Kaunti ya Mombasa inavyoendeshwa.

Hatua hii inajiri baada ya kuenea uvumi kuwa Awiti hatawania kiti cha ugavana na badala yake kuwa naibu gavana, jambo alilolipinga na kulikanusha.

Awiti alisisitiza kuwa atagombea kiti hicho chini ya chama cha Wiper.

Wakati huo huo, Seneta wa Mombasa Hassan Omar pia ameweka wazi nia yake ya kugombea kiti cha ugavana wa Mombasa mwaka ujao.

Omar alisema kuwa chama chao cha Wiper kimejipanga vilivyo kuongoza nchi hii na watakuwa na mpeperushaji bendera wa chama hicho Kalonzo Musyoka kwenye kinyanganyiro cha kuelekea ikulu.

Hatua ya Omar kutaka kuwania kiti cha ugavana inajiri baada ya wafuasi wake wengi kumtaka kuwania wadhfa huo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kauli ya Omar iliungwa mkono na naibu mwenyekiti wa chama hicho Mutula Kilonzo Junior, ambaye alisema kuwa wafuasi wa Wiper wamekuwa wakiunga mkono viongozi wengine tangu mwaka wa 2007 na sasa ni wakati mwafaka wao kusimama kivyao ili kuongoza taifa hili.