Shirika la Mzalendo Trust lilifanya utafiti na kuwataja baadhi ya wabunge ambao tangu wachaguliwe hawajawahi kuchangia mijadala bungeni.
Shirika hilo linalohusika na kufuatilia utendekazi wa bunge la kitaifa lilitoa orodha ya wabunge 27 wanaodaiwa kuwa kimya bungeni licha ya wenzao kuchangia mijadala inayowahusu wananchi wao.
Mbunge wa Nyali Hezron Awiti na mwenzake wa Likoni Masoud Mwahima ni miongoni mwa wabunge waliodaiwa kuwa mwaka wote wa 2015 hawakutoa hoja yoyote kuhusu maswala yanayowakumba wananchi katika maeneo yao.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Mombasa waliotoa maoni mbalimbali kuhusu orodha hiyo inayoendelea kuzua hisia tofauti katika mitandao na vyombo vya habari.
“Wamefanya vizuri sana kutoa hayo majina kwa sababu sasa wabunge wataanza kushtuka na kuchangamka. Wamezoea kwenda bungeni bila kuongea lolote wakati mwananchi wanaumia,” alisema Silas Oloo, anayefanya biashara ya kuuza nguo.
Baadhi ya wakaazi walipinga swala hilo kwa kusema kwamba sio lazima mbunge achangie mada bungeni, na kuongeza kuwa utendekazi mzuri wa mbunge ni kutokana na miradi wanayofanyia watu.
“Mbunge anaweza kuongea sana bungeni lakini ukiangalia watu wake bado wanateseka. Sio wote tumejaliwa maneno ya kuongea kwa hivyo tusiwalaumu wabunge wote jameni,” alisema mkaazi wa Mombasa.
Wabunge wengine wa ukanda wa pwani waliotajwa katika orodha hiyo ni mbunge wa Kinango kaunti ya Kwale Gonzi Rai na Gideon Mung’aro wa Kilifi Kaskazini.