Malumbano ya kisiasa kati ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho na Mbunge wa Nyali Hezron Awitti yameonekana kuchacha huku Awitti akimkosoa Joho kwa kudai kuwa Gavana huyo anaeneza siasa za uchochezi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika eneo bunge lake Nyali mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mbunge huyo wa Nyali alisema kuwa Gavana Joho aliweka bayana kuwa wanaostahili kuchaguliwa kama viongozi katika kaunti hiyo ni watu halisi wa kaunti hiyo ya Mombasa na wala sio watu wa kutoka maeneo mengine ya nchi.

Awitti alisema kuwa kila Mkenya ana uhuru wa kupigania wadhfa wowote ule wa uongozi katika eneo lolote lile la nchi hivyo basi uchochezi kama huo kamwe haufai kuenezwa na Kiongozi kama Joho.

Awitti alihoji kuwa siasa za uchochezi zinazoendelezwa na Gavana huyo wa kaunti ya Mombasa kamwe hazina msingi wowote na ni lazima hatua zifaazo zichukuliwe dhidi ya Kiongozi huyo.

“Tunashangazwa na kiongozi kama Joho kusema kuwa watu wa Mombasa wachague mtu wa kutoka Mombasa na wajitenge na viongozi wa kutoka maeneo mengine ya nchi hiyo ni uchochezi mkubwa”,alisema Awitti.

Hata hiyo, Gavana Joho alieonekana kujitenga na tetesi hizo na kutotamka lolote kuhusiana na madai ya Awitti, huku Awitti akishikilia wazi kuwa atambwaga Joho katika kinyang’anyiro cha ugavana wa kaunti ya Mombasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.