Wamiliki wa baa katika eneo la Likoni wamepewa makataa ya siku 21 kuafikia matakwa ya sheria za Halmashauri ya kupambana na dawa za kulevya nchini, Nacada.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu kamishna wa eneo bunge la Likoni Albert Mureithi amesema haiwezekani kwa eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya baa zinazouza pombe kwa wakaazi, pasi kuwa na vibali vya kuendesha biashara hiyo.

Mureithi amesema kuwa miongoni mwa sheria ambazo baa hizo zimeonekana kukiuka ni pamoja na kukosa leseni za kuendesha biashara hiyo, pamoja na matakwa mengine ambayo ni lazima kila anayemiliki sehemu ya kuuzia pombe aweze kutimiza kwa mujibu wa sheria kutoka halmashauri ya Nacada.

Mureithi alisema kuwa eneo hilo lina jumla ya baa mia tatu na kati ya hizo ni thelathini na mbili pekee ambazo zimetimiza sheria hizo, huku zilizosalia zikiendesha biashara hiyo kinyume cha sheria.

OCPD huyo aidha ameongeza kuwa kuna baadhi ya baa ambazo zinauza pombe duni ambayo haijathibitishwa na mamlaka ya kudhibiti ubora wa bidhaa nchini KEBS.

“Ikiwa wanaomiliki baa hizo watakosa kuafikia sheria hizo ndani ya kipindi cha siku ishirini na mmoja, basi itawalazimu maafisa wa usalama kukagua baa hizo moja baada ya nyengine ili kutathmini zile zitakazokuwa zimekiuka sheria za Nacada,” alisema Mureithi.

Aidha, aliwaonya vijana ambao hawajahitimu umri wa miaka kumi na minane wanaotumia vileo kwa kusema kuwa atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria.