Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya maskwota katika shamba lenye utata la Waitiki katika eneo bunge la Likoni, Kaunti ya Mombasa wanatishia kususia shughuli ya utoajia wa hati miliki inayotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii.

Maskwota hao walidai kuwa serikali haina mpango wa kuwasaidia bali inataka kuwanyanyasa, wakitaja hatua ya kutozwa pesa kama kizingiti kikubwa.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika eneo la Likoni, maskwota hao walisema kuwa hali yao ya kiuchumi haiwezi kuwaruhusu kulipa shilingi elfu 182 ili kupata vibali hivyo.

“Sisi hatuwezi kulipa hiyo pesa. Kama watatupa hati miliki watupe na kama hawataki watuache tukae,” alisema mwanamke mmoja aliyekataa kujitambulisha.

Maskwota hao pia wanasema kuwa wamekaa hapo kwa muda mrefu na kwamba hawana mahali pa kwenda, na hivyo wanashangazwa na utaratibu wa serikali kuwatoza pesa, jambo ambalo wanasema sio la kawaida.

“Hakuna mahali Kenya hii ambapo maskwota wanalipia hati miliki na sisi tunashangaa kwanini sisi tulipie,” aliongeza mama huyo.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza shughuli hiyo siku ya Jumamosi, na hatua ya maskwota hao kutishia kususia linatia wasiwasi iwapo zoezi hilo litafaulu.