Baadhi ya walimu wa shule za umma hasa za upili wamejitokeza kupinga vikali hatua ya waziri wa elimu nchini kupiga marufuku likizo fupi kwa wanafunzi wa shule za umma.
Haya yanajiri mda mchache tu baada ya waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kupiga marufuku likizo fupi na shughuli za kuwatembelea wanafunzi wa bweni shuleni kwenye muhula wa tatu kama njia mojawapo ya kukabiliana na visa vya wizi wa mitihani.
Kwenye mahojiano na baadhi ya walimu mjini Nyamira, wengi wao wamepinga hatua hiyo wakisema kuwa huenda hali hiyo ikachangia katika kuongezeka kwa visa vya wizi shuleni.
"Inakuwaje kwamba waziri Matiang'i anaweza piga marufuku likizo fupi kwa wanafunzi wa shule za umma ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanafunzi hao hupata nafasi ya kununua bidhaa muhimu wanaporejea nyumbani kwa likizo fupi na iwapo hilo litatekelezwa visa vya wizi shuleni vitaongezeka," alisema James Omari.
Kwa upande wake Michael Nyakang'i ambaye ni mwalimu wa shule moja katika kaunti hiyo alisema kuwa hatua ya wanafunzi kunyimwa likizo fupi itawanyima wanafunzi hao nafasi ya kutangamana na wazazi wao.
"Kwangu mimi naona kama hii hatua ya waziri Matiang'i inahujumu haki za wanafunzi kwa maana ni vizuri wanafunzi hao kupewa nafasi ya kutangama na wazazi kabla yao kuketi kuifanya mitihani ya kitaifa," alihoji Nyakang'i.