Baada ya vyombo vya habari kuangazia matatizo ya hedhi kwa wanafunzi wa kike, baadhi ya shule kwenye Kaunti ya Kisumu zimeanza kupata afueni baada ya wahisani kujitokeza kutoa misaada wa sodo kwa wanafunzi wao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wa kike wa Shule ya Upili ya Achar ilioko eneo la Otonglo katika Kaunti ya Kisumu walifaidika na msaada wa sodo uliotolewa kwao na mhisani Milkah Ochiel anayefanya kazi na shirika moja la kijamii katika eneo hilo linalojulikana kama Child Suport Home Based Centre.

Akiwa mshirikishi mkuu wa shirika hilo katika eneo la Nyanza, Ochiel alitoa sodo pakiti 300 zikiwemo na sabuni kwa zaidi ya wanafunzi 250, bidhaa ambazo ziligharimu Sh40,000.

Akihutubu wakati wa kusambaza bidhaa hizo, mshirikishi huyo alihoji kuwa ukosefu wa sodo kwa wanafunzi wa kike kwenye shule nyingi eneo la Nyanza umekuwa tatizo sugu kwa kisomo cha wanafunzi hao.

“Wanafunzi wengi wametatizika na kuathirika kimasomo baada ya kukaa nje mara kwa mara kila mwezi kwa kukosa bidhaa hizi za kujisitiri wakati wa hedhi,” alisema Ochiel.

Aidha, Ochiel alisema kuwa shirika lake limeapa kusimama na shule za eneo hilo ili kuokoa masomo ya wanafunzi wa kike na kuahidi kurai mashirika mengine na wadhamini pamoja na washikadau kushikana mikono kuokoa elimu ya mtoto msichana.

Wanafunzi wengi hujikuta kwenye njia panda wakati wanapokua kwenye nyakati zao za hedhi, wanapolazimika kutegemea misaada ya marafiki wao wa kiume ambao huwaahidi kuwapa usaidizi kabla ya kuwashirikisha kwenye mapenzi, ambayo baadaye mimba za mapema, kuacha shule na kupata magonjwa ya zinaa kutibuka.