Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wakazi wa Mombasa wametoa ombi la kutaka kuhusishwa katika miradi ambayo serikali inapania kuanzisha ili kuonyesha uwajibikaji na kujali maslahi yao.

Haya yanajiri huku wengine wao wakionyesha kutofurahishwa kwao kuhusiana na uzinduzi wa barabara moja katika mji huo ambayo ilipewa jina la mwanawe kiongozi wa Cord Raila Odinga, mwendazake Fidel Odinga.

Wakiongeo siku ya Jumatano pindi tu baada ya kuhutubiwa na Odinga kwenye eneo la Nyali jijini Mombasa, wakazi hao waliitaja hatua hiyo kuwa mbaya wakidai kuwa kuna mashujaa wengi katika eneo la Pwani ambao wamefanya mambo mengi ya kutajika na ingekuwa vizuri iwapo waliohisika katika mpango huo.

Bakari Mwamdoe, ambaye aliongea kwa niaba ya wakazi hao aliwashtumu baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Pwani kwa kuhusika kwenye uamuzi ambao mara nyingi unaleta mkanganyiko kwa wakazi.

Aidha aliwataka viongozi kuwaheshimu wenyeji sababu wao ndio wanawapa nafasi hiyo ya kuongoza, hivyo basin ni vyema zaidi kufanya mashauriano mwafaka na kutimiza maamuzi kamili.

“Tunawaomba viongozi wetu kuzingatia wenyeji mwanzo kabla ya kufanya maafikiano yoyote yale, sababu sisi ndio waajiri wao, si vibaya kuipa jina kama hilo lakini wakazi wa eneo husika sharti washauriwe,” alisema mwenyeji huyo.