Mipango ya mazishi ya mhudumu wa bodaboda kaunti ya Nakuru imesalia kuwa kitendawili baada ya babake mwenye umri wa miaka 99 kumkana katika mahakama moja ya Nakuru.
Mzee Benjamin Kibiwott Chesulut (mwalimu mstaafu) kupitia kwa wakili wake Steve Biko, alimwambia Jaji Sila Munyao kwamba marehemu aliyeaga akiwa na umri wa miaka 46 hakuwa mtoto wake halisi.
Hivyo basi alisema kwamba hakuwa tayari kumzika katika shamba lake la ekari 100 lililoko Keringet, Molo.
Wilson Kerich Kibiwott ambaye alifariki mnamo Februari 15 baada ya kuhusika katika ajali barabarani karibu na mji wa Molo alipangiwa kuzikwa nyumbani kwao Molo wiki mbili zilizopita.
Mwenda zake amekuwa akiishi na mamake pamoja na bibi yake nyumbani kwao Molo.
Babake marehemu alifika kortini akidai kwamba bibi yake na watoto wengine walikuwa wakiishi bila idhini na kimakosa katika shamba lake.
Tofauti zilizuka katika familia hiyo kuhusu mahali pa kuzikwa baada ya babake kumkana mwanawe pindi tu alipofariki huku akisema hakuwa amemwoa mamake kulingana na mila na desturi za jamii ya Kikalenjin.
Kibiwott, ambaye ameoa bibi watano alisema kwamba Kerich hakuwa mtoto wake na hivyo basi hakuwa na sababu ya kulazwa katika shamba lake.
Bi Chelagat, hata hivyo alikanusha madai ya mumewe akisema kwamba yeye na wanawe walikuwa wameishi mahali hapo kwa zaidi ya miaka 30 baada ya kuolewa na Mzee Kibiwott.
Vilevile alisema kwamba Mzee Kibiwott ndiye aliyewapa shamba hilo kwani alikuwa bibi wake wa tatu na kwamba alizaa watoto watano naye.
Kibiwott alisisitiza kwamba anataka uchunguzi wa DNA kufanywa ili kubaini ukweli.
Mzee huyo ambaye pia ni meneja mstaafu wa kampuni ya Kirobon ilyoko viungani mwa mji wa Nakuru ni mmiliki wa mashamba mengine ya zaidi ya ekari 300 katika maeneo ya Ngata na Subukia ambapo familia zake zingine zinaishi.
Mwili wa marehemu umekuwa ukihifadhiwa katika ufuo wa hospitali kuu ya wilaya ya Molo huku familia yake ikingojea mahakama kutatua swala hilo.