Katibu mkuu wa chama cha Ford Kenya Kaunti ya Mombasa Yassir Bajaber amesema kuwa mrengo wa upinzani haufai kutumia jina la NASA katika uchaguzi ujao.
Bajaber alisema kuwa jina hilo jipya la NASA hauna umaarufu na haujulikani na Wakenya wengi.
Katibu huyo mkuu alisema iwapo upande wa upinzani unataka kushinda katika uchaguzi wa Agosti, sharti utumie jina la mrengo wa Cord, ambao unajulikana kote nchini.
“Cord ndiyo maarufu kuliko NASA, itakuwa bora iwapo hatutatumia NASA wakati wa uchaguzi mkuu ujao,” alisema Bajaber.
Aidha, alisema kwamba itakuwa vigumu kuanza kuuza sera za muungano wa NASA kwa wananchi, ikizingatiwa kwamba uchaguzi mkuu umekaribia sana.
“Itakuwa vigumu kuanza kuuza sera za NASA ikizingatiwa kuwa uchaguzi utafanyika baada ya miezi michache,” alisema Bajaber.
Wakati huo huo, amewataka viongozi wakuu wa upinzani kuelewana mara moja na kuchagua mgombea atakayepeperusha bendera katika uchaguzi mkuu.
“Itakuwa bora iwapo tutaanza kumpigia debe mapema kinara atakaye teuliwa na viongozi hao,” alisema Bajaber.