Waziri wa utalii nchini Najib Balala amezitaka serikali za kaunti kushirikiana vyema na wadau nchini ili kuboresha sekta hiyo.
Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa maeneo ya kuegesha meli za kigeni, Balala alisema ushirikiano bora ndio njia pekee ya kuendeleza sekta ya utalii na uchumi wa taifa.
Balala aidha aliwataka viongozi kujitenga na siasa zitakazo sambaratisha sekta hiyo na badala yake kushirikiana vyema katika maswala ya kimaendeleo.
Alisema kuwa sekta hiyo imeimarika hadi asilimia 60 kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka humu nchini na hata mataifa ya kigeni.
“Tunatarajia kupokea watalii zaidi kutoka mataifa ya kigeni hususan msimu huu wa mwezi wa Disemba,” alisema Balala.
Wakati huo huo, Balala alisema kwamba serikali itashirikiana na mataifa mengine ili kuboresha zaidi sekta ya utalii.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Bandari nchini KPA Catherine Mturi amewahimizi watalii kuondoa wasiwasi wa kuzuru sehemu mbalimbali nchini,kwa kuwa usalama umeimarishwa.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema atashirikiana na wadau kuhakikisha viwango vya utalii vinaimarika katika kaunti hiyo na kote nchini kwa jumla.