Balozi wa marekani humu nchini Bw Robert Godec alifanya ziara maalum mjini Mombasa, ziara inayoonekana kurejesha uhusiano mwema baina ya taifa la Kenya na lile la Marekani.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo ya siku ya Jumanne, Godec aliyashukuru mataifa yote mawili kwa kushirikiana kukabili ugaidi, ikizingatiwa kwamba Mombasa ni mji ulioathirika zaidi na tatizo hilo.
“Kumekuwa na mabadiliko na usalama umeimarika hasa hapa Mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla. Hiyo ndio sababu nilikuwa wa kwanza kutangaza kuondolewa kwa marufuku ya usafiri kwa wananchi wa Marekani waliokuwa na nia ya kuzuru eneo hili,” alisema balozi huyo.
Vile vile, balozi huyo alisema kwamba Marekani itaendelea kushirikiana na taifa hili katika maswala ya usalama na maendeleo, na kusema kwamba uhusiano kati ya nchi hizi mbili umedumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho aliyeandamana na balozi huyo alisema kwamba mji huo umeendelea kupokea watalii wengi tangu serikali ya marekani ilipoondoa marufuku hiyo.