Mwenyekiti wa halmashauri ya Bandari nchini KPA, Marsden Madoka amesema kuwa halmashauri hiyo inatafuta uungwaji mkono kutoka kwa wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii ili kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari, Madoka amesema kuwa mikakati ya ujenzi wa eneo rasmi la kuegesha meli za kitalii inaendelea ili kuona kuwa swala la utalii nchini linaimarishwa zaidi na kuwavutia wageni wengi.

Amesema kuwa juhudi za idara ya usalama nchini kwa ushirikiano na mataifa ya magharibi kukabiliana na maharamia katika bahari hindi ya Pwani ya Somalia na Kenya kumesaidia pakubwa kuimarisha uchumi wa nchi kupitia kuzuru kwa meli za kitalii nchini.

Madoka ameitaka serikali kupunguza ushuru unaotozwa meli za kitalii zinapoingia nchi kama njia moja wapo ya kuvutia meli nyingi za kitalii, akisema kuwa hatua hiyo itaimarisha biashara na uwekezaji mkubwa nchini.

"Tunataka serikali kuangalia swala hili kwa kina na kuweza kuwapunguzia wamiliki wa meli za kitalii ada ya ushuru ili kuvutia meli nyingi za kitalii na kuimarisha sekta hiyo sambamba na kukuza uchumi wa nchi," alisema Madoka kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne.

Meli zengine za kitalii zinatarajiwa kuwasili katika bandari ya Mombasa kuanzia mwezi wa Septemba hadi Disemba huku usimamizi wa bandari hiyo ukidai kutenga shilingi milioni 100 kugharamikia ujenzi wa sehemu ya kupokea watalii wanapowasili katika bandari hiyo ya Mombasa.