Wakaazi wa mitaa ya Kaptembwa na Githima, mjini Nakuru wana wingi wa matumaini, kutokana na barabara inayoendelea kujengwa kupitia mitaa hiyo, huku wakisema kuwa mradi huo utafungua sehemu hiyo kwa maendeleo.

Share news tips with us here at Hivisasa

 “Tuko na uhakika ya kwamba barabara hii itakapomalizika, miradi mingi ya maendeleo itachipuka sehemu hii na hali ya maisha itaimarika,” anasema Shadrack Anida, ambaye kando na kufanya biashara ya uchukuzi wa bodaboda, ana kibanda cha kuuzia vyakula ambacho mke wake hukishughulikia katika mtaa wa Kaptembwa.

Barabara hiyo ambayo inaanzia kutoka barabara kuu ya Nakuru-Eldoret karibu na kiwanda cha Eveready, inapitia kando ya mtaa wa Githima na Kaptembwa.

Mradi huu uko chini ya serikali ya Kaunti ya Nakuru, na umefadhiliwa na Serikali kuu ya Kenya pamoja na Benki ya Dunia.

Barabara hii ndiyo awamu ya kwanza ya mradi huu, ambao unanuiwa kuimarisha huduma kwa wakazi wa vitongonji, kwa kuleta huduma kama vile barabara, vinjia vya miguu, mitaro ya maji taka, taa za usalama (mulika mwizi) na afya kwa jamii.

Awamu ya pili itahusisha kuwekwa lami kwa barabara inayotoka Githima hadi mto Ndarugu, na ya tatu ni ukarabati wa barabara inayopita katikati ya soko la Kaptembwa hadi mtaa wa Pondamali.

Kampuni tatu ambazo ni Golden Cara, Nyoro Construction Company na Jet Builders and Construction ndizo zilizo na kandarasi ya mradi huu.

Hata hivyo, baadhi ya wenyenji wanalalamikia kasi ya chini ambayo inatumika kuendesha mradi huu.

Dereva mmoja wa matatu za Shabab Line ambaye hubeba abiria kutoka mjini hadi Kaptembwa kupitia Githima aliwataka wenye kandarasi kuharakisha mradi huu.

“Wanafanya kazi nzuri lakini mwendo wao uko chini sana. Ingelikuwa kampuni ya Mchina ndiyo yenye hii kandarasi, kazi yenyewe ingekuwa inaelekea kuisha,” alilalamika dereva huyu.