Baraza la magavana limetakiwa kushauriana na serikali badala ya kuendelea kushinikiza kuwepo kwa kura ya maamuzi.
Wito huu umetolewa na mbunge wa Molo Jacob Macharia, ambaye ametoa wito kwa viongozi kushirikiana na kutekeleza majukumu yao bila kutofautiana kama ilivyoshuhuduwa mwaka jana.
Mbunge huyo amesema mdahalo wa kuwepo kwa kura ya maamuzi unaoendelezwa na baraza la magavana pamoja na vigogo wa muungano wa demokrasia na mageuzi CORD, umeweka nchi katika mazingira ya uchaguzi, huku viongozi pamoja na wananchi wakiendelea kutofautiana kuhusiana na wito huo.
Macharia amewataka viongozi wanaopendekeza kuwepo kwa kura hiyo kufanya mashauriano na serikali, ili kupata suluhu la masuala wanayoyapigania badala ya kuanza kampeini za mapema.
Haya yanajiri wakati ambapo mwenyekiti wa baraza la magavana Isaac Ruto amesisitiza kwamba hawatasita kushinikiza kuwepo kwa kura ya maamuzi, baada ya kukutana na wahusika wa serikali katika makongamano mawili bila mafanikio.
Kwa mujibu wa gavana Ruto, maeneo ya Mashinani yanakumbwa na changamoto nyingi zinazohitaji uimarishwaji wa miundo msingi, na kwamba hilo litafanyika iwapo fedha zinazotengewa serikali za kaunti zitaongezwa hadi asilimia 45 ya bajeti ya kitaifa kila mwaka.