Baraza la wazee la Wamiji limesema litaandaa mchakato wa kumchagua atakayegombea kiti cha ubunge eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada ya kubainika kuwa mbunge wa sasa Masoud Mwahima anayumbayumba kimrengo baada ya kuonekana kujiunga na mrengo wa Jubilee.

Baraza hilo ambalo linaaminika kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa eneo hilo limesema sasa itawalazimu kuchagua kiongozi ambaye watakuwa na imani naye.

Baraza hilo lilidai kuwa Mwahima ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama inavyotakikana kikatiba, na badala yake kukimbilia mrengo wa Jubilee kama maficho, ili kupata tiketi ya kuwania kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Mshirikishi wa baraza hilo Ali Mwasirima amesema wakazi wengi wa Likoni wanakabiliwa na matatizo si haba.

“Kulingana na ahadi Mwahima alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita, anastahili kufikia sasa awe amesaidia angalau robo ya vijana wa eneo hili kupata ajira kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo. Kufikia leo hakuna chochote kilichofanywa na afisi ya mbunge huyo kwani anakiri kuwa miradi mingi imetekelezwa na serikali chini ya usimamizi wa Jubilee,” alisema Mwasirima.

Akitoa mfano wa vijana waliojisalimisha kutoka kundi la kigaidi la al-Shabaab, Mwasirima alisema ilikuwa ni ahadi ya mbunge huyo kuwapeleka vijana hao kufanyiwa ushauri nasaha ila kufikia sasa hakuna lolote lililofanywa.

Alisema kuwa iliwalazimu wazee hao kuomba msaada kwa mshirikishi mkuu wa kanda ya Pwani Nelson Marwa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Baraza hilo Bwana Salim Mwavumo alisema kuwa wananchama wanatarajiwa kuandaa mkutano wa kumtangaza rasmi atakayejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho cha ubunge wa Likoni.