Hujambo Daktari Matiang’i.
Imenibidi kama mwanahabari anayejali maslahi ya mzazi kukaa kitako na kutunga barua hii.
Natumahi u buheri wa afya ulipo, huko Nairobi.
Hapa Kisii tunapunga upepo mwanana japo kwa machungu.
Wakati ulichukua hatamu ya kuiongoza wizara ya elimu, wazazi wamekuunga mkono na hata katibu mkuu wa chama cha KNUT amekiri kupendezwa na kazi yako.
Umeonekana ukipanga safari za ghafla kwa baadhi ya shule nchini Kenya, Hatua ambayo imeanza kubadilisha huduma katika shule za serikali.
Matiang’i wewe ni mzaliwa wa Kisii, na ukweli ni kwamba nyumbani kunaungua.
Walimu wa shule za upili kutoka kaunti ndogo ya Marani kaunti ya Kisii hawasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
Duru za kuaminika zinasema kuwa, wazazi wanalia usiku kucha wakisema laiti Matiang’i angefahamu tunayoyapitia.
Kwa sasa sina mengi ila tu ujumbe wangu kwako ni huu. Juzi umeonekana kwa vyombo vya habari ukikemea walimu ambao huwanyanyasa wazazi kwa hela zisizo na maana, Ukakiri kuwachukulia hatua.
Tumeshuhudia ukiwafuta kazi baadhi ya walimu wakuu wanaozembea kazini , hatua ambayo wazazi wameipongeza kwa mikono miwili.
Bwana matiangi hili ni swali linalohitaji jibu la dharura. Je, pesa wanazodaiwa wazazi wa kaunti ndogo ya Marani na walimu wakuu wa shule za upili shilingi 1500 ili Wanafunzi kufanya mtihani wa Muigo (mock) ni za kazi gani?