Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amepinga madai kwamba chama cha ODM kitawapa baadhi ya wagombea tiketi ya moja kwa moja.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza wakati wa kutoa fedha kwa makundi ya wanawake na vijana katika eneo hilo, Bedzimba amesema viongozi wote ambao wana lengo la kuwania nyadhifa tofauti kupitia chama cha ODM lazima wachaguliwe na wananchi kupitia mchujo.

“Kila mmoja atakwenda kwa mchujo na hiyo ndio demokrasia,endapo hulitaki hilo basi una fursa ya kuwania kiti kama mgombea wa kibinafsi,” alisema Bedzimba.

Haya yanajiri baada ya Ali Mbogo, ambaye ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge Kisauni kudai kuwa kinara wa ODM Raila Odinga alimahidi tiketi ya moja kwa moja.

Akizungumza na wanahabari katika Shule ya msingi ya Bamburi siku ya Jumanne, Mbogo alidai kuwa waliafikiana hayo na Raila katika ziara yao ya pamoja nchini Ujerumani wiki mbili zilizopita.

Aidha, amedai kuwa huenda kusiandaliwe kura ya mchujo katika eneo bunge hilo, na badala yake kuandaliwe kura ya maoni kujua mgombea yupi wa ODM ndiye maarufu zaidi katika eneo hilo.