Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba ametoa wito kwa wakaazi kutoka kanda ya Pwani kumuunga mkono Gavana wa Mombasa Hassan Joho katika azma yake ya kuwania urais mwaka 2022.
Bedzimba amesema Gavana Joho ana rekodi nzuri ya maendeleo tangu alipokuwa mbunge wa eneo hilo katika kipindi cha mwaka 2007-2013, hivyo basi anapaswa kuungwa mkono ili kuongoza taifa.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika uwanja wa Shule ya msingi ya Kisauni Baptist, mbunge huyo alitoa mfano wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mbunge wa Gatundu, akisema alifikia wadhfa wa urais baada ya kuungwa mkono na wenyeji kutoka eneo la Kati.
“Nataka kuwaambia watu wa Pwani lazima mumlinde na kumuenzi kiongozi wenu ambaye ameonyesha ushupavu na kupata sifa ya kitaifa. Huyu ndiye mtu tutakayeunga mkono 2022. Tunataka tupate mtu atakaye tugawia keki,” alisema Bedzimba.
Mbunge huyo alisema kuwa wakati mwafaka umefika kwa eneo la Pwani kupata mtu atakayepeperusha bendera ya rais, na kumtaja Joho kama atakayefikia azma hiyo.
Haya yanajiri baada ya Joho ambaye ni naibu kiranja wa chama ODM kutangaza wazi azma yake ya kuwania urais mwaka 2022.