Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amewarai wakaazi wa kaunti ya Mombasa kuwaunga mkono vinara wa mrengo wa upinzani nchini Cord, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula kushinikiza kuvunjwa kwa Tume ya IEBC.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Bedzimba alisema kuwa tayari Wakenya wamechoshwa na jinsi tume hiyo inavyopanga zoezi la uchaguzi mkuu.

Aidha, mbunge huyo alisema kuwa huenda kukashuhudiwa wizi wa kura iwapo tume hiyo itasalia mamlakani.

Bedzimba alisema kuwa lazima tume hiyo ivunjwe na makamishna wengine wanaojali maslahi ya wananchi na taifa zima kuchaguliwa.

Alisisitiza kuwa mrengo wa Cord hautakubali matokeo ya uchaguzi mkuu ujao iwapo makamishna hao hawatabanduliwa.

"Tafadhali ndugu zangu tuunge mkono chama chetu cha Cord na hawa jamaa wa IEBC tuwaondoe ili tufanye uchaguzi wa haki,” alisema Bedzimba.

Mbunge huyo wa Kisauni pia aliwakosoa maafisa wa usalama wanaowashambulia wakati wanapofanya maandamano ya amani, kwa kusema kuwa lazima hali hiyo isitishwe.