Huku waumini wa dini ya Kiislamu wakiendelea kufunga katika mwezi wa Ramadhan kote ulimwenguni, wafanyibiashara wa tende wanalalamikia ongezeko la bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya jumla.
Wakizungumza katika Soko la Marikiti mjini Mombasa, wafanyibiashara hao walisema kuwa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuondolewa kwa ushuru ya bidhaa hizo wakati huu wa Ramadhan, bado hakuna lolote ambalo limefanywa ili kuona kwamba bei ya bidhaa hiyo inashuka.
Kulingana na Idi Maalim, muuzaji wa bidhaa za Futar katika soko hilo, bei ya tende katika masoko ya jumla haijateremka.
Maalim alisema kuwa hali hiyo inawafanya wengi kutoka jamii maskini kukosa kununua bidhaa hiyo kama ilivyo desturi kwa Waislamu kuanza kula vyakula kama hivyo kabla ya kujumuika na wenzao kwenye sala ya magharibi.
Mfanyibiashara huyo alisema kuwa hatua hiyo haijawaathiri wanaohitaji bidhaa hiyo pekee yao, bali pia wao kama wafanyibiashara kwani mara nyingi huandikisha hasara kwa kuwa tende hukosa soko kama ilivyokuwa hapo awali.
Muuzaji wa tende katika duka la jumla eneo la Mwembe Tayari Issa Mzee, alisema kuwa walitarajia amri iliyotolewa na Rais Kenyatta kufuatwa ila kufikia sasa hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa ili kuondoa ushuru wa bidhaa hiyo.
Ameitaka serikali kufuatilia mchakato wa namna bidhaa hiyo inavyosafirishwa hapa nchini ili kutekeleza azimio la serikali.