Seneta mteule Beth Mugo ameutaka mrengo wa Cord kukoma kueneza uvumi kwamba serikali ya Jubilee ina mpango wa kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, Mugo alisema madai hayo ni porojo tu.
Mugo amewataka viongozi wa upinzani kusitisha uvumi huo kwani huenda ukazua vurugu na fujo miongoni mwa wananchi.
Seneta huyo alisema sharti upande wa upinzani ushirikiane vyema na serikali ili kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu unatekelezwa katika njia ya amani, wala sio kuwagawanya Wakenya katika misingi ya kisiasa.
Mugo amewataka viongozi humu nchini kuendeleza ushindani wao wa kisiasa bila chuki za dini na ukabila, huku akihimiza Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kujitenga na siasa za vyama ili kuwe na uchaguzi wa huru na haki.
Wakati huo huo, amewataka wakaazi wa Mombasa na ukanda wa Pwani kwa ujmla kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kusajili wapiga kura linaloendelea kote nchini.