Mwakilishi mteule wa walemavu katika bunge la kaunti ya Nakuru Emma Mbugua amesema kuwa unyanyapaa na ubaguzi katika jamii bado ni changamoto kubwa kwao.
Akiongea mjini Nakuru alhamisi wakati wa kuadhimisha siku ya walemavu kote duniani katika bustani ya Nyayo, Mbugua amezitaka familia zilizo na walemavu kutowaficha kwa hofu ya kukejeliwa na jamii.
Kulingana na mwakilishi huyo, inahitaji moyo kukaa na walemavu manyumbani kwani watadhoofika wakati wanatengwa hata na wale ambao wanastahili kuwapa upendo.
“Wengine ni walemavu wa macho, wengine miguu, mikono, kuna wale ambao wanahitaji watu wa kuwaongoza, kuna wale ambao uti wa mgongo umevunjika, wengine wanaugumu wa kufikiri na kuelewa mambo kwa haraka. Tukiwadharau kwa sababu ya hali hiyo, ni nani atawasaidia?” alihoji Mbugua aliyeteuliwa kutoka eneo bunge la Bahati.
Vile vile alitoa changamoto kwa serikali za kaunti kuwapa elimu walemavu akisema ukosefu wa elimu unachangia unyanyapaa huo.
“Mimi nimepata kutangamana na vikundi vya akina mama kutoka Naivasha ambao waliungana baada ya watoto wao kupata magonjwa na kulemaa wakiwa wadogo, lakini kwa sababu ya kutowaficha na kujikubali, wameweza kuwasaidia watoto wao kupitia matibabu na mazoezi hata kujipatia chakula,” akasisitiza Mbugua.