Baada ya biashara ya uchukuzi wa pikipiki maarufu kama bodaboda kuendelea kunoga nchini, umaarufu wake umekita katika baadhi ya miji na kumiminikiwa na vijana.
Kazi hii ambayo katika miaka ya awali ilionekana kuwa duni miongoni mwa wananchi, leo imekuwa maarufu zaidi na hata kuwa miongoni mwa kazi bora ambazo zinakimu maisha ya wengi ikiwemo wazee pamoja na vijana.
Dominic Wanyama ni mwendeshaji bodaaboda ambaye kazi hii imemlisha kwa zaidi ya miaka tisa sasa. Anasema kuwa kazi hii imekuwa kama dhahabu miongoni mwa vijana hali ambayo imesababisha kubuniwa kwa sheria na masharti pamoja na kanuni za utendakazi.
''Mwanzoni kazi hii haikupendwa na wengi na kila mtu alikuwa na uhuru wa kubeba abiria katika eneo lolote. Lakini leo ni sharti ijulikane kila mtu steji ambayo anafanya kazi,'' Wanyama alisema Alhamisi.
Katika maeneo mengi pembeni mwa nchi, makundi mengi ya bodaboda hujibandika majina na kila mwanachama wake kupewa nambari ya huduma ambapo kokote aendako hutambuliwa kama mwanachama wa kundi fulani kutoka eneo fulani.
Hali ya fujo na vurumai imekuwa ikishuhudiwa katika baadhi ya steji za bodaboda mjini Kisumu kutokana na hali ya baadhi ya wahudumu kukosa kujitambulisha maeneo wanayotoka na vikundi wanavyo hudumu chini yake.
Jambo hili limetokea wakati wahudumu hao wanapoendeleza kampeni za kupiga vita walaghai ambao wamekuwa wakipaka tope kazi hiyo kwa kuwaibia wateja, na kumaliza kabisa wizi wa pikipiki ambapo wahudumu wa bodaboda waliuawa kwa wingi na kunyang'anywa pikipiki zao awali.