Wamiliki wa hoteli Pwani wamesema kuwa wameanza kushuhudia kuimarika kwa biashara hasa msimu huu ambapo wageni wengi wanazuru eneo hilo kwa likizo ya mwezi Agosti.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, mwenyekiti wa muungano wa wamiliki wa hoteli Pwani, Sam Ikwaye, alisema kuwa hoteli nyingi ambazo zilifungwa kati ya mwezi Mei na Julai kufuatia kushuka kwa biashara tayari zimefunguliwa.
“Hoteli nyingi tayari zimefurika na wageni na bado tunatumai kuwa biashara itaimarika hata zaidi kwani watalii kutoka mataifa ya kigeni tayari wameanza kuwasili nchini,” alisema Ikwaye.
Amesema kuwa hatua hiyo inatokana na kuimarika kwa hali ya usalama nchini ikilinganishwa na mwaka uliopita wakati sawia na huu, ambapo mataifa ya kigeni yaliwawekea raia wake vikwazo vya kuzuru nchini kutokana na hofu ya usalama.
“Mwaka uliopita tulipata hasara kubwa sana. Wengi wa wageni tuliokuwa nao walikuwa wale wa humu nchini. Mataifa mengi ya Ulaya mfano Ufaransa, Marekani, Uingereza ambao ndiyo hututembelea kwa wingi walituwekea vikwazo,” alisema Ikwaye.
“Hata hivyo kwa sasa hali ni shwari hasa baada ya mataifa hayo kuyaondoa marufuku haya ya usafiri na kuwaruhusu raia wake kuzuru nchini kwa kuwa serikali imeimarisha usalama,” aliongeza.
Hata hivyo, Ikwaye ameeleza hofu yake kuwa joto la kisiasa linaloshuhudiwa nchini kwa sasa huenda likaathiri sekta ya utalii, hasa wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.
“Kwa kawaida mwaka wa uchaguzi na baada ya uchaguzi huwa kunashuka idadi ya wageni wanaozuru nchini kwa hofu kuwa huenda kukatokea mgawanyiko hasa kutokana na yale yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007,” alisema Ikwaye.