Wamiliki wa hoteli katika ukanda wa Pwani wanakadiria kushuka kwa biashara hasa kipindi hiki ambapo kunashuhudiwa idadi ndogo ya watalii wanaozuru eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa Muungano wa Wahudumu wa Hoteli Pwani, Sam Ikwaye, alisema kuwa maeneo ya Malindi na Watumu ndiyo yameathirika zaidi ambapo takribani asilimia 40 ya hoteli tayari zimefungwa.

“Tangu msimu wa Pasaka kutamatika, hoteli nyingi hapa Pwani zimerekodi idadi ndogo ya watali ikiwa ni kati ya aslimia 35-40. Hali hii tayari imefanya wengine kufunga biashara zao,” alisema Ikwaye.

Kulingana na Ikwaye, huenda idadi kubwa ya wafanyikazi wa hoteli katika eneo hilo wakapoteza ajira kutokana na kushuka kwa mapato iwapo hali hiyo itaendelea hadi mwezi Agosti.

“Wafanyikazi wengi wapo katika hatari ya kupoteza ajira. Ikiwa hakuna wageni wa kuhudumiwa, hakuna mwajiri atakaye kubali kugharamia malipo bila kazi,” aliongeza Ikwaye.

Ikwaye alisema kuwa hali hii hutokana na kutokuwa na safari za ndege za kuwaleta watalii katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwani kipindi hiki watalii wengi hurudi katika mataifa yao baada ya kumalizika kwa lizikizo ya siku kuu ya Pasaka.

Aidha, alisema kuwa hali hii hushuhudiwa kila mwaka kati ya mwezi wa Aprili na Agosti.