Maduka mengi ya kuuza nyama mjini mombasa haswa katika soko la Marikiti yameonekana kutowatosheleza wateja baada ya nyama zilizokuwa kwenye majokofu kuisha kufikia saa nne asubuhi kufuatia sherehe za sikukuu ya Eid zinazoendelea kote duniani.
Wakaazi wengi waliokuwa wamefika kununua bidhaa hiyo wamelazimika kusubiiri kwenye foleni ndefu iliyoanza kushuhudiwa tangia saa kumi asubuhi.
Kwa mujibu wa muhudumu wa duka moja katika soko hilo, Abdulrahim Hussein, imemlazimu yeye mwenye kukocha kiasi cha nyama alichokuwa ameweka ili kusherehekea pamoja na familia yake hadi pale wasambazaji wa nyama kutoka kichinjio cha Mariakani walipoleta mali nyengine ambayo pia anasema imeisha mwendo wa saa nane mchana.
Aidha kwa upande wake mama Njeri anayeuza mboga pamoja na vioungo vya vyakula mbalimbali katika soko hilo, amekiri kuwa wakati huu ndio ambao wafanyabiashara wengi katika soko hilo hupata soko kwa wingi.
Hata hivyo kulingana na mteja mmoja Salim Khassim aliyekuwa kwenye foleni akisubiri kununua nyama, amewaomba wafanyabiashara wa soko hilo kununua mali nyingi zaidi msimu huu wa sikukuu kwani familia zote hapa kisiwani hutegemea soko hilo kwa bidhaa ya nyama.