Maafisa wa mamlaka ya ushuru nchini KRA na KPA wameharibu bidhaa zinazodaiwa kuingia humu nchini kupitia bandari ya Mombasa kwa njia ya magendo ikiwemo sukari, mchele na kemikali aina ya spiriti.
Bidhaa hizo zinazodaiwa kumilikiwa na kampuni ya ‘Compact Freight System’ na ‘Auto port’, kampuni inayomilikiwa na familia ya Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano katika Bandari ya Mombasa kunakotekelezwa shughuli hiyo ya uharibifu wa bidhaa hizo, kwa Niaba ya Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Ushuru nchini KRA John Njiraini, kamishna wa uwakala wa forodha na udhibiti wa mipaka nchini Julius Musyoki amesema kuwa makasha 19 alipatikana na sukari ghushi huku 49 akipatikana na Michele na kemikali hiyo.
Musyoki amesema kuwa makamishna wa KRA pamoja na viongozi wengine serikalini wanaendelea na majadiliana huko jijini Nairobi na ripoti kamili kuhusu wamiliki wa bidhaa hizo wanaokabiliwa na sakata hiyo ikitarajiwa kutolewa.
"Tumechukua jukumu la kuharibu bidhaa hizi ili iwe funzo kwa wengine kama hawa wenye kuingiza bidhaa humu nchini ka njia ya kimagendo na lazima biashara hiyo kusitishwa," alisema Musyoki.
Kamishna huyo amewaonya wafanyibiashara wanaoingiza bidhaa na kutoa katika bandari ya Mombasa kuwa waangalifu na bidhaa wanazoleta na kuhakikisha kuwa wanalipa ushuru jinsi inavyohitajika ili kuona kuwa uingizaji wa bidhaa za magendo unasitishwa katika bandari hiyo ya Mombasa.