Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Sheikh Abubakar Bini amesema kuwa Mamlaka ya kupambana na pombe haramu na mihadarati Nacada, inaudhaifu wa kutekeleza majukumu yake.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Bini alisema kuwa wananchi hutozwa kodi ya kiasi kikubwa ili kuiwezesha mamlaka kama hiyo kutekeleza wajibu wake.

Alisema kuwa ni vyema kwa mamlaka hiyo kufuatilia utaratibu ufaao katika kuhakikisha kuwa wamepambana na mihadarati vilivyo.

Aidha, Bini amependekeza mamlaka hiyo kufanyiwa mageuzi na kutaka viongozi wa dini kushirikishwa katika vita dhidi ya pombe haramu nchini.

Alisema kuwa hatua hiyo ndiyo itakayo iwezesha mamlaka hiyo kuangamiza janga la mihadarati na pombe haramu kabisa.

Aidha, kiongozi huyo alikashifu ufisadi unaoendelea katika mamlaka hiyo na kusema kuwa kanda ya Pwani imeathirika sana na utumizi wa mihadarati na pombe haramu, huku takwimu zikionyesha vijana wengi wameathirika.