Biwi la simanzi lilitanda katika kijiji cha Gekonge eneo bunge la Mugirango Kaskazini baada ya wenda zao Geoffrey Kamonde na Jemima Kamonde kuzikwa baada ya kuawa wiki moja iliyopita na washukiwa wa uhalifu. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye hafla hiyo ya mazishi siku ya Jumatano, mbunge wa eneo hilo Charles Geni alitishia kuandaa maandamano ya pamoja na wakazi wa eneo hilo hadi kwenye ofisi za kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga ili kushinikiza kuhamishwa kwake. 

"Hatuwezi kaa huku tukiangalia wananchi wasio na hatia wakiuliwa, na ndio sababu nimepanga kuandaa maandamano ya pamoja hadi kwenye afisi ya kamishna Onunga ili kushinikiza kuondolewa kwake," alisema Geni. 

Geni aidha alisema maafisa wa polisi wanawafahamu wahalifu wanaowahangaisha wakazi katika eneo hilo huku akiwataka maafisa hao kuweka mikakati ya kuwatia mbaroni washukiwa wa uhalifu ili wakabiliwe kisheria.

"Ninachofahamu ni kuwa maafisa wa polisi wanawafahamu wahalifu wanaowahangaisha wakazi wa eneo hili na sharti wachukue jukumu la kuwahakikishia wakazi usalama wao kwakuwatia mbaroni washukiwa," alisema Geni.

Ikumbukwe kuwa kwa muda sasa visa vya uhalifu vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo mengi katika kaunti ya Nyamira bila ya idara ya usalama kuweka mikakati ya kukabiliana na visa hivyo.